Bunge la Kenya lililokarabatiwa na ambalo
limekuwa gumzo kubwa kwa sababu ya gharama ya viti vya bunge hilo, hatimaye
limefunguliwa rasmi na rais wa nchi hiyo Mwai Kibaki.
Viti hivyo vimegharimu dola 3,000 za
kimarekani kwa kila kiti kimoja vikiwa jumla ya 350 vimetengenezwa na kitengo
cha magereza nchini humo.
Zabuni ya kwanza ya kutengeneza viti hivyo
ilitolewa kwa kampuni moja ya nje lakini ilifutwa baada ya baadhi ya wabunge
kugundua kila kiti kingegharimu dola 5000 za kimarekani.
Maafisa wanasema ukarabati huo uliogharimu
dola milioni 12 utaliweka bunge katika mfumo mpya wa kisasa wa komputa.
"Mabadiliko tunayoyafanya yataleta
mabadiliko chanya katika uongozi," spika wa bunge Kenneth Marende
ameiambia BBC.
Amesema mfumo wa kupiga kura wa elektroniki
utawawezesha wabunge kupiga kura kwa uhuru wao binafsi kuliko kulazimika kupiga
kura kwa kuhofia vyama vyao.
"sasa mbunge atakuwa peke yake, huru
kabisa binafsi, atafanya maamuzi yake na kubonyeza tu kitufe."
Viti vya Bunge la zamani la Kenya
Mwandishi wa BBC Odeo Sirari mjini Nairobi,
anasema baadhi wanaona viti hivyo kuwa ni vya gharama kubwa sana kuliko mabunge mengine katika jumuiya ya
madola.
Waziri mkuu wa Kenya
Raila Odinga na rais Mwai Kibaki pamoja na wabunge ni miongoni mwa wanaolipwa
mshahara wa juu sana barani Africa.
Wabunge walifurika katika jengo hilo lililokarabatiwa
wakati rais na spika wakiongoza utaratibu wa sherehe za ufunguzi.
Ukarabati huo ulianza mwezi Aprili mwaka
2010 na ulikuwa umepangwa kuchukua mwaka mmoja kumalizika lakini ulichelewa
kwasababu ya utata ulioghubika zabuni yake, mwandishi wetu anasema.
Mbunge John Mbadi, katika kamati ya
uwekezaji aliongoza upinzani juu ya zabuni ya kwanza.
"hatukuweza kuelewa ni kwa vipi
wabunge wangekuwa wanakaa katika viti vinavyogharimu karibu shilingi 400,000 za
Kenya kama dola 5,000, ambazo kwa kiwango chochote cha kawaida zingeweza
kujenga nyumba kwa wananchi kadhaa," ameiambia BBC.
"ilikuwa ni upuuzi," amesema.
Mwandishi wetu anasema watu wengi
wamelalamika kuwa gharama za sasa bado ni juu.
David Langat, anayesimamia uzalishaji
katika magereza nchini Kenya, amesema vifaa vyote vilivyotumika vilitoka nchini
Kenya lakini gharama za viti
zimekuwa kubwa sana.
Ameiambia BBC kuwa viti hivyo vyenye uzito
wa kilo 50 kila kimoja vina kinga dhidi ya moto na vina dhamana ya miaka 30.
Kwa sasa Kenya ina jumla ya wabunge 220
lakini ukumbi huo umewekwa viti 350 idadi ambayo watachaguliwa katika uchaguzi
ujao mwezi Machi kwa mujibu wa katiba mpya.
chanzo:BBC