Mgogoro ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
umeingia katika sura mpya baada ya viongozi wake wawili waandamizi,
Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo
kuuandikia uongozi wa chama hicho wakitaka uikane taarifa inayowachafua
mitandaoni.
Zitto na Dk Mkumbo wanatuhumiwa kupokea fedha na
kushirikiana na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa na wale wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kuivuruga Chadema.
Taarifa hiyo yenye kichwa cha habari `Ripoti ya
siri juu ya Zitto Kabwe’, ambayo imesambaa katika mitandao mbalimbali ya
kijamii katika siku za karibuni inadaiwa kuwa iliandaliwa na Kitengo
cha Upelelezi cha Chadema baada ya uchunguzi wa mwenendo wa Zitto ndani
na nje ya nchi kuanzia mwaka 2008.
Sehemu ya taarifa hiyo ya mtandaoni inadai kuwa
Zitto alipelekewa kiasi cha Dola za Marekani 266,000 (Sh416 milioni)
huko Ujerumani na maofisa wa Usalama wa Tanzania, Desemba 16, 2009.
Ripoti hiyo inadai kuwa fedha hizo zilipitishwa
katika Benki ya Berliner ya Ujerumani kwenye akaunti ya raia wa nchi
hiyo, Andrea Cordes, ambaye anadaiwa kumpelelekea Zitto.
Taarifa zaidi zinadai kuwa fedha hizo ziligawiwa kwa wafuasi mbalimbali wa chama hicho na miongoni mwao ni Dk Mkumbo.
Zitto amlima barua Dk Slaa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana,
Zitto alisema amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod
Slaa kumwomba athibitishe ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ kama ni ya kweli
au chama hicho kiikanushe ili aweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
waandishi wa kile alichokiita ‘hekaya.’
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho
(chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008
hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema,” alisema Zitto kwenye taarifa
yake.
Zitto alisema taarifa hiyo ni ya kutunga na
iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imemfedhehesha, imemsikitisha na
kumkasirisha.
Alisema taarifa hiyo iliibuliwa katika kipindi
ambacho alikuwa ziarani barani Ulaya katika nchi za Uswisi na Uingereza
ambako alikuwa anafuatilia fedha zilizofichwa na Watanzania katika nchi
hizo.
“Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka
kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka
Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo
waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu,” alieleza
Zitto katika taarifa yake.--soma--www.mwananchi.co.tz